Washington imesema ubalozi bandia wa Marekani ambao umekuwa ukiendesha shughuli zake kinyume cha sheria nchini Ghana kwa takriban muongo mmoja umefungwa.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa, ubalozi huo bandia umekuwa ukiendeshwa na magenge ya wahalifu katika mji mkuu wa Ghana, Accra kwa muda wa miaka 10.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shughuli za ubalozi huo zimekuwa zikiendeshwa na shakhsia mbali mbali raia wa Ghana na Uturuki wakiwemo mawakili, ambao wamekuwa wakitoa viza na vyeti vingine ghushi kwa wananchi wa Ghana.
Habari zaidi zinasema kuwa, washukiwa kadhaa raia wa Uturuki wanaozungumza Kiingereza na Kiholanzi ambao wamekuwa wakihudumu katika ubalozi huo bandia wamekamatwa.
Aidha makumi ya viza halisi na bandia zimepatikana katika ofisi za ubalozi huo wa Marekani nchini Ghana, mbali na paspoti 150 za nchi 10 tofauti, vipakatalishi, simu kadhaa za rununu na vyeti vingine ghushi.
Inaarifiwa kuwa, ubalozi huo ulikuwa unaitisha dola elfu 6 za Marekani, ili kupeana kitambulisho bandia cha Marekani, viza au cheti cha kuzaliwa cha Marekani.
Maafisa usalama nchini Ghana walivamia jengo la ghorofa mbili lililokuwa na ofisi za ubalozi huo bandia katika mji mkuu Accra hivi kariuni, baada ya kupokea taarifa za kijasusi kutoka ubalozi halali wa Marekani nchini Ghana.
0 on: " Ubalozi feki wa Marekani nchini Ghana wafungwa baada ya miaka 10 "