Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za serikali nchini Kenya leo wamefanya mgomo wakitaka kutimizwa makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 kati ya muungano wao na serikali kuhusu kuongezwa mishahara na kuboreshwa mazingira ya kufanyia kazi.
Polisi wameshuhudiwa wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya madaktari, wauguzi, na wafamasia ambao waliandamana hadi makao makuu ya Wizara ya Afya jijini Nairobi.
Madaktari hao waliokuwa wamevalia mavazi meupe na kofia za kijani zinazotumika katika vyumba vya upasuaji baadaye walielekea pia katika makao makuu ya Wizara ya Fedha jijini Nairobi. Muungano wa Madaktari na wauguzi Kenya ambao una wanachama wapatao elfu tano umeeleza kuwa, makubaliano hayo ya malipo yalipasa kuwapatia nyongeza ya mshahara ya asilimia 300, kujadili mazingira yao ya utendaji kazi na mifumo ya kazi, kuangalia upya vigezo vya kupandishwa cheo na kutatua tatizo la uhaba wa wafanyakazi wa huduma za afya mahospitalini.
Samuel Oroko, Mkuu wa Muungano wa Madaktari wa Kenya amesema kuwa waliipatia serikali muda wa kutosha kutekeleza makubaliano hayo na kwamba mazungumzo yanapasa kufikia ukomo. Amesema madaktari wataendelea kugoma hadi makubaliano hayo yaliyopewa jina la CBA kwa kifupi yatakapotekelezwa.
Wagonjwa wameshuhudia wakiwa wamekwama katika hospitali kadhaa nchini Kenya bila ya kupatiwa matibabu.
![]() |
Wagonjwa wakiwa katika hospitali ya Thika Level Five wakiwa wamekata tamaa baada ya madaktari kuanza mgomo |
0 on: " Madaktari Kenya wagoma, polisi yatumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya "