Kundi la kigaii la al Shabab limezidisha mashambulizi yake katika maeneo ya umma na yenye idadi kubwa ya watu nchini Somalia
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita pekee kundi hilo limeshambulia bandari kubwa ya Mogadishu na kuua watu karibu mia moja. Mashambulizi hayo yamezusha wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa vitongoji vya mji wa Mogadishu.
Kundi la al Shabab ambalo ni tawi la kundi la kigaidi la al Qaida katika eneo la mashariki mwa Afrika, liliundwa na wanachama waliojitenga na Muungano wa Mahakama za Kiislamu hapo mwaka 2006 na kuanzisha vita dhidi ya serikali ya wakati huo ya Somalia kwa kisingizio cha kuanzisha utawala wa Kiislamu.Takwimu zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha muongo mmoja wa kuanzia 2006 hadi 2016 kundi la al Shabab limefanya mashambulizi 364 ya kigaidi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kundi la kigaidi la al Shabab linasaidiwa kifedha na kijeshi na Eritrea, japokuwa serikali ya Asmara inakanusha madai hayo.
Baada ya kuasisiwa, kundi hilo liliteka maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Somalia. Hata hivyo Disemba 2012 jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika lilifanikiwa kuwafukuza wapiganaji wa al Shabab katika bandari muhimu ya Kismayo na mjini Mogadishu. Kufurishwa katika maeneo hayo muhimu kulipunguza kwa kiwango fulani uwezo na ushawishi wa kundi hilo la kigaidi. Vilevile kutimuliwa Mogadishu na katika maeneo mengine muhimu ya kistratijia kulilifanya kundi la al Shabab lianzishe mashambulizi ya kulipiza kisasi hususan katika nchi za Kiafrika zilizotuma askari wa kulinda amani nchini Somalia. Miongoni mwa mashambulizi hayo ni yale yaliyolenga kituo cha kibiashara cha Westgate jijini Nairobi na Chuo Kikuu cha Garisa ambayo yameua mamia ya watu na shambulizi la kigaidi la Kampala wakati wa mechi za soka za Kombe Dunia mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini. Vilevile kufurushwa kundi la al Shabab katika maeneo na ngome zake muhimu kulikata vyanzo la pato vya kundi hilo.
Kundi la al Shabab ambalo wakati wa kuasisiwa kwake lilifanikiwa kusajili vijana wengi wa Kisomali kwa ahadi za kurejesha amani na utulivu nchini humo, katika miaka ya hivi karibuni limeshindwa na kupata pigo katika jitihada za kusajili wapiganaji wapya. Pamoja na hayo bado linadhibiti baadhi ya maeneo ya vijijini na limekuwa likifanya mashambulizi ya kuvizia na kujilipua kwa mabomu katika maeneo ya mijini.
Kwa sasa kundi la al Shabab limezidisha mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya umma na yenye idadi kubwa ya watu mijini katika kipindi hiki ambapo serikali ya Somalia inajitayarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 28 Disemba. Mashambulizi hayo yanafanyika kwa shabaha ya kukwamisha zoezi hilo muhimu la kidemokrasia. Inatarajiwa kuwa uchaguzi wa 28 mwezi huu nchini Somalia utasaidia kutayarisha mazingira ya kuundwa serikali kuu imara katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikisumbuliwa na machafuko ya ndani na migogoro ya kisiasa tangu miongo miwili iliyopita.
0 on: " al Shabab yaendelea kua tishio nchini Somalia "