![]() |
Mfalme Charles Mumbere |
Mfalme wa Uganda anayekabiliwa na mashtaka ya ugaidi amekubaliwa kuwa na mpishi binafsi na 'Fridge' ndogo kwenye chumba chake korokoroni. Amri hii imetolewa na mahakama. Charles Mumbere, Mfalme wa Rwenzururu amekubaliwa kupata huduma hii kwa sababu za kiafya; anaugua shinikizo la damu na kisukari.
Hata hivyo mamlaka za Uganda zimesema mfalme huyo hatakubaliwa kuwa na mpishi kutoka nje. Mfalme Mumbere alikamatwa mwezi uliopita baada ya maafisa wa usalama kuvamia Kasri lake Magharibi mwa Uganda wilaya ya Kasese. Zaidi ya watu 80 waliuawa kwenye makabiliano hayo.
Kiongozi huyo wa kijamii amekanusha kuhusika na ghasia hizo. Alikamatwa pamoja na wafuasi wake 150 waliojumuisha walinzi wake. Wakili wake, Caleb Alaka ameambia BBC kwamba lazima maafisa wa jela waheshimu uwamuzi wa mahakama. Alaka amesema wapishi wengi wa mfalme waliangamia wakati wa uvamizi huo. Mfalme huyo atakubali mpishi atakayesajiliwa na maafisa wa jela.
Hata hivyo kumetokea na taarifa kwamba vyumba vya gereza havina umeme wala eneo la kuweka 'Fridge'. Mfalme huyo anazuiliwa katika jela kuu la Luzira mjini Kampala. Haijabainika ikiwa mashtaka ya ugaidi yanahusisha operesheni ya kijeshi iliyofanyika Kasri lake au mauaji ya afisa wa polisi hapo mwezi Machi.Mfalme huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena tarehe 28 mwezi Machi mwakani.
Serikali ya Uganda imelaumu Ufalme wa Rwenzururu ulioko wilaya ya Kasese kwa kuwasajili na kutoa mafunzo kwa wapiganaji wakiwa na nia ya kujiondoa kutoka kwa Uganda na kuunda taifa lao huru kwa jina Yira.
Eneo hilo lililoko katika mpaka wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekumbwa na ghasia kati ya jeshi na makundi yenye silaha. Makabiliano hayo yamesababisha mauaji ya wanajeshi na hata raia. Kabla ya kutawazwa Mfalme, Charles Mumbere aliishi kwa miaka mingi nchini Marekani, ambapo alihudumu katika nyumba ya wazee jimbo la Pennsylvania
0 on: " Mfalme wa Uganda kupata mpishi Jela "